Recent Posts

Simu FEKI 600,000 Zazimwa.....TCRA Yaendelea Kusaka Zingine


Uzimaji wa Imei bandia ulifanyika usiku wa kuamkia jana kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika simu zaidi ya 600,000 zenye Imei batili. 

Kwa mujibu wa TCRA, Imei ni namba ya kimataifa ya utambuzi wa vifaa vya kielektroniki, ikiwamo simu. Ina tarakimu 15 ambazo ni za kipekee kwa kifaa husika na zinatambulika kimataifa. Namba hizo hutumika kudhibiti bidhaa bandia au simu kutumiwa na mtu mwingine. 

Jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alisema takwimu hizo ni zile ambazo zimetokana na kazi ya kukata mawasiliano katika simu bandia iliyofanyika kuanzia saa sita usiku mpaka saa kumi alfajiri ya jana. 

Alisisitiza kuwa mtambo huo unaendelea na kazi kuhakikisha kuwa hata simu ambazo hazipo au hazikuwa hewani zitakapowashwa hazitafanya kazi. 

“Kazi ya kuzima simu hizo ilianza usiku wa kumkia jana saa sita usiku na kila kampuni ya mtandao wa simu ilipaswa kuzima simu za wateja wake ambazo ni feki na kazi ya mtambo ni kuhakikisha simu iliyozimwa inapowekewa kadi ya mtandao mwingine haifanyi kazi na kuhakikisha simu zote feki zitakazoingia nchini hazifanyi kazi,” alisema Mungy. 

Hata hivyo, kuna baadhi ya wamiliki wa simu ambao walitilia shaka ufanisi wa mtambo huo kwa madai kuwa tayari walishathibitishiwa na TCRA kwamba simu zao ni feki, lakini bado zinafanya kazi. 

“Simu yangu mimi niliangalia nikaambiwa ni feki na niibadilishe kabla ya tarehe 16 Juni, lakini jana wamezizima feki ya kwangu bado inafanya kazi kama kawaida napiga na kupokea simu kama zamani,” alisema Nael Joseph. 

Kuhusu suala hilo, Mungy alisema: “Hoja hizo zimejitokeza kwa wingi na wengine walifikia hatua ya kuushutumu mtambo wetu kuwa ni feki na kuwa umeshindwa kuzima simu feki ukazima orijino, lakini ukweli ni kwamba mtambo ule hauzimi kama taa au kama ule uliozima matumizi ya analojia bali unazima taratibu. 

"Niweke sawa kwamba mtambo huu hauonei mtu na unazima simu zote zilizo feki.” 

Mungy aliongeza kuwa wengi wamekuwa hawaelewi mantiki ya ujumbe wa uthibitisho.Alisema ujumbe unamtaka mmliki wa simu kuoanisha jina linalotajwa kama ndilo jina halisi la simu yake. “Kama jina linalotajwa na Imei linaoana na lililoandikwa kwenye simu yako, basi sio feki, lakini majina yakiwa hayafanani ndipo simu inakuwa feki,” alifafanua. 

Vodacom wazungumza 
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia alisema walipewa jukumu la kuzima simu feki za wateja wao na TCRA.

“Jana saa sita usiku tulitekeleza agizo kama lilivyotolewa na TCRA na inavyoonekana wengi wao walikuwa wamejipanga kwani simu nyingi zimezimwa, lakini baadhi wamerejea hewani japokuwa wapo ambao mpaka sasa hawajarudi,” alisema Mworia . 
Simu FEKI 600,000 Zazimwa.....TCRA Yaendelea Kusaka Zingine Simu FEKI 600,000 Zazimwa.....TCRA Yaendelea Kusaka Zingine Reviewed by praise joe on 21:28 Rating: 5

No comments:

Theme images by i-bob. Powered by Blogger.